Waandamanaji wanaopinga utawala wa Rais Pierre Nkurunzinza leo wameanza siku mbili za kusitisha maandamano yao katika barabara za mji mkuu wa Burundi, Bujumbura ambayo yamekuwepo kwa zaidi ya mwezi mmoja. Barabara za mji huo leo zilishuhudia hali ya utulivu na maduka kadhaa yalifunguliwa huku askari wakionekana kushika doria kwa utulivu. Hapo jana, washambuliaji walilishambulia soko lililoko katikati ya mji huo kwa maguruneti na kuwaua watu watatu na kuwajeruhi wengine 40. Kiongozi wa asasi ya kiraia Pacifique Nininahazwe ametangaza watasitisha maandamano ya kupinga azma ya Nkurunziza kuwania muhula wa tatu madarakani wikiendi hii ili kuwezesha watu kuwazika kwa heshima wale waliopoteza maisha yao wakidai demokrasia na kuahidi kwamba maandamano hayo yatarejea tena kwa kishindo Jumatatu.